Latest News 14 Jul 2022
Waziri wa Uganda asifu uwekezaji wa Tanzania katika Ziwa Victoria.
Waziri wa Uchukuzi wa Uganda Mhe. Byamukama Fred amesifu uwekezaji unaoendelea kufanywa na Serikali ya Tanzania katika kurahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam na kupita katika Reli ya Kisasa na hatimaye kubebwa na Meli katika Ziwa Victoria na kufika bandari ya Port Bell nchini Uganda.
Mhe.Byamukama alisema kuwa Serikali ya Tanzania imeshatayarisha kila kitu kwaajili ya Waganda huku akitoa mifano ya ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza pamoja na ukarabati wa meli ya mabehewa ya MV Umoja na kusisitiza kuwa miradi hiyo ina thamani ya mabilioni ya hela, hali iliyopelekea kuiamsha Serikali ya Uganda ili iweze kurekebisha miundombinu ya bandari zake.
“Kwa ukarabati na ujenzi wa meli mpya, mizigo yetu haitakwama tena, na kama wanajumuiya ya Afrika Mashariki, kama hizi nchi mbili zinaweza kufanya biashara, hata wanajumuiya wengine wanaweza kufanya biashara, nimefurahi katika mipango ya Tanzania kuwa hawatafanya biashara na Uganda pekee bali watafanyabiashara na nchi nyingine za Afrika Mashariki.”
Akielezea umuhimu wa ujio wa Waziri huyo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli Philemon Bagambilana amefurahishwa na kitendo cha Serkali ya Uganda kufika Mwanza na kuojionea maendeleo ya miradi na uwekezaji wa Serikali katika kuboresha miundombinu ya usafiri katika ushoroba wa kati.
“Kuna vitu tumeongea, kwa mfano tumeona kuna umuhimu wa kufanya maboresho katika miundombuni kwa maana ya bandari zetu kusudi ziweze kupokea meli kubwa zinazokuja hasa za kubeba makasha (containers), amejionea na amefurahi na kupongeza na ameahidi kwamba Serikali ya Uganda pia itakwenda kufanya juhudi za namna hiyo kusudi hizi juhudi zetu ziweze kuleta tija.”
Akiongea katika ziara hiyo ya siku moja (06.07.2022) Katibu Mtendaji wa Shirika la Ushoroba wa Kati (CCTTFA) Flory Okandju alisifu jitihada za Serikali ya Tanzania za kujenga miundombinu ya usafiri na ya kurahisisha biashara, na kuwaita wafanyabiashara wa Uganda na Watanzania pamoja na Wakongo kuitumia miundombinu hiyo ili kukuza uchumi kati ya Tanzania na Uganda na hatimae kufukuza umasikini na kuongeza ajira katika nchi hizo.