Latest News 02 Oct 2025

MV. LIEMBA KUONDOA ADHA YA USAFIRI MWAMBAO WA ZIWA TANGANYIKA
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) Mej.Gen Mst. John Mbungo amewahakikishia wananchi wanoishi katika mwambao wa Ziwa Tanganyika na nchi za Jirani zinazopakana na ziwa hilo kuwa mara tu baada ya meli ya MV. Liemba itakapokamilisha ukarabati wake itakuwa ikisafirisha abiria na mizigo yao katika bandari mbalimbali zilizopo katika ziwa hilo.
Ameseyasema hayo tarehe 11.09.2025 alipotembelea mradi wa ukarabati wa meli ya MV. Liemba katika Bandari ya Kigoma akiwa ameambatana na timu ya wataalamu kutoka TASHICO inayoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Ndg. Eric Hamissi.
“Mara meli hii ukarabati wake utakapokamilika itakuwa moja ya mchango mkubwa sana katika ziwa hili la tanganyika ambapo Serikali itakuwa inatoa huduma kwa wananchi kwa kuwasafirisha wao kama abiria na mizigo yao pembezoni mwaa bandari nyingi zilizomo katika ziwa hili, hii ni pamoja na kufika katika nchi Jirani ya DR Congo na Zambia,” Alisema.
Awali wakati akielezea maendeleo ya ukarabati wa meli hiyo Meneja Mradi Mhandisi Elias Kivara alisema kuwa meli imefikia asilimia 32 ya utekelezaji huku akisisitiza kuwa kazi nyingi zisizohitaji meli kuwa kwenye chelezo zipo katika hatua za mwisho kumalizika na kuongeza kuwa wanatarajia kupokea Injini mbili, majenereta manne vifaa vingine vya umeme pamoja na vifaa vya uendeshaji mwezi Oktoba, 2025.
Akifafanua kazi zilizofanyika Mhandisi Kivara alisema “Kazi zilizokamilika ni replate, kuweka vyuma upya sehemu zilizoharibika kwenye eneo la Nahodha,eneo la vyumba vya abiria,vyoo, mabafu pamoja na eneo la mgahawa, kwa ujumla kazi hizi ambazo hazihitaji meli kuwa kwenye chelezo zinatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba na kubakia na kazi zinazohitaji meli kupanda kwenye chelezo”
Halikadhalika alifafanua kuwa meli hiyo inabadilishwa mfumo wa mabomba, mfumo wa umeme na mfumo wa uendeshaji na kusema kuwa mifumo ya maji safi na maji taka tayari imeshafikia hatua za mwisho kumalizika.
Pia alisema kuwa kazi inayoendelea ni pamoja na kuondoa rangi ya zamani na kuweka rangi mpya katika maeneo mengi ya meli hiyo ambapo kazi hiyo imeshafanyika katika maeneo ya juu ya meli (upper deck) eneo la katika kati (main deck) pamoja nae neo la injini na hivyo kubakiwa na maeneo ya matenki na eneo la mizigo ambayo hadi kufikia mwezi Oktoba itakuwa kazi imemalizika.
“Katika upande wa machinery (mitambo) tunatarajia mwezi Oktoba kupokea injini mbili ambazo tayari zimeshafanyiwa majaribio, pamoja na majenereta manne, mawili makubwa na saidizi mawili pamoja na (navigational equipment) vifaa vya uendeshaji, kitu kitakachokuwa kimebakia ni shaft na propellor ambavyo vinatarajiwa kufika mwezi Disemba, 2025 kwahiyo tunatarajia mradi huu kuisha kwa wakati”.
Katika taarifa yake Mhandisi Kivara alisema kuwa baadhi ya changamoto zilizopelekea mradi kuchelewa tangu kuanza kwake tarehe 13 Julai 2024 ni pamoja na kuchelewa kuwasili kwa mahitaji katika hatua za awali hali iliyopelekea hadi sasa kuwa na asilimia chache za utekelezaji, maji ya ziwa kujaa na kusababisha meli kushindwa kupanda kwenye chelezo ili kuweza kutoa shaft na propellor na hivyo kuendelea na kazi ndogo ndogo wakiendelea kusubiri.
Ukarabati wa Meli ya MV. Liemba yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 200 za mizigo unafanywa na Mkandarasi M/S Brodosplit JSC ya nchini Croatia kwa kushirikiana na Dar es Salaam Merchant Group (DMG) ya nchini Tanzania na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai,2026.