Latest News 02 Oct 2025

News Images

MABAHARIA WA MT SANGARA WAKUMBUSHWA MAJUKUMU YAO

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Meli Tanzania Ndg. Eric Hamissi amewakumbusha mabaharia wa meli ya MT. Sangara kuendelea kuilinda na kuitunza meli hiyo inayofanya safari zake kati ya Bandari ya Kigoma, Tanzania na Bandari ya Kalemie, DR Congo.

Ameyasema hayo leo tarehe 09.09.2025 wakati alipofika katika Bandari ya Kigoma kuwapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya lakini pia kuona utendaji wa kazi wao wakati wakijiandaa kuanza safari ya kuelekea Bandari ya Kalemie, nchini DR Congo.

Sambamba na pongezi hizo Ndg Eric aliwakumbusha mabaharia hao kuwa makini na utunzaji wa vifaa vya meli hasa eneo la injini huku akisisitiza kuwa kumekuwa na tabia ya mabaharia kujificha kwenye upya wa chombo na hivyo kubaki kuangalia tu usalama wa chombo bila ya kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kuangalia utimamu wa chombo upande wa mitambo mbalimbali.

“Mara nyingi sana watu wanazembea wanajificha kwenye ule upya wa vyombo, sasa havichukui muda kusumbua kwasababu haviangaliwi, ninaomba sana kuwe na ukaguzi wa mara kwa mara wa hizi meli, itakuwa ni jambo la aibu sana hizi meli zianze kuaharibika kwasababu hazikuangaliwa wakati Serikali imewekeza fedha za kutosha kuzirudisha hizi meli katika upya, ni kama mmepewa kitu kipya kabisa, nawaombeni muitunze” Alisema.

Hata hivyo, Ndg. Eric aliwakumbusha kutodharau taarifa za hali ya hewa huku akisisitiza kuwa ni bora kukaa na mzigo wa mteja kwa siku mbili ama tatu ili kulinda usalama wa chombo lakini pia usalama wa mabaharia hao.

“Naomba msidharau taarifa za hali ya hewa, nafahamu kua mna uzoefu lakini kama kuna taarifa zinasema kuna hali ya hewa mbaya, acheni msiende, lakini yakitokea mkiwa njiani basi mtatumia umahiri wenu lakini huwezi kulazimisha kwenda wakati unaona hali ni mbaya. Hali ya hewa inapokuwa mbaya tafuteni mahala pa kujihifadhi. Hata ukikaa na mzigo wa mteja kwa siku mbili tatu kwa usalama wa meli fanyeni hivyo, mvitunze hivi vyombo ili Serikali iendelee kutupa fedha Zaidi, nawaombeni hilo,” Ndg. Eric Alisisitiza.

Kwa upande wake Nahodha wa Meli ya MT. Sangara Naho. Titus Mnyanyi amemshukuru Mkurugenzi kwa kuwapa motisha ya kufanya kazi zaidi na kuahidi kuongeza juhudi ya kazi ili waweze kui nua mapato ya TASHICO.