Latest News 02 Oct 2025

MV NEW MWANZA YAFANYA SAFARI YA KWANZA MWANZA KWENDA BUKOBA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo tarehe 21 Septemba, 2025 ameshuhudia safari ya kwanza ya meli ya MV New Mwanza kutoka Bandari ya Mwanza Kusini iliyopo jijini Mwanza kuelekea Bandari ya Bukoba ikiwa imebeba wataalamu kutoka kwa Mkandarasi, Maafisa wa Serikali na wawakilishi kutoka vyombo vya ulinzi na usalama.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kushuhudia tukio hilo la kihistoria Mhe. Mtanda amesema kuwa kukamilika kwa meli hiyo ni juhudi za Serikali chini ya Rais Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kuimarisha sekta ya usafiri na kuwahakikishia wananchi wa Mwanza na Ukanda wa Ziwa Victoria usafiri wa uhakika.
“Wananchi wa Mwanza na kanda ya ziwa wamepata usafiri wa uhakika kwani Mhe. Rais Samia amedhamiria kuwaondoka kwenye adha ya ajali zilizotokana na matumizi ya usafiri duni wa mitumbwi na kwamba nauli zitakua nafuu sana kwa safari za ndani na nje ya nchi.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TASHICO Ndg. Eric Hamissi amebainisha kuwa Ujenzi wa meli hiyo umefikia asilimia 99 na baada ya safari hiyo ya kutoka Bandari ya Mwanza Kusini kuelekea Kemondo hadi Bandari ya Bukoba wanatarajia kupata majibu ya ufanisi wa kitaalamu kabla ya kuanza safari zake katika Ziwa Victoria.
"Kwa mara ya kwanza Meli hii itafika Bandari ya Bukoba na italala huko na kesho itarejea Mwanza na ni lazima tumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani ameikuta ikiwa na 40% tu ya ujenzi mwaka 2021 huku zikiwa zimelipwa Tshs. Bilioni 36 pekee lakini amemalizia fedha zote na kukamilisha Shilingi Bilioni 120." Alisema Eric.
“Meli hiyo yenye urefu wa mita 92.6 ambao unakaribia urefu wa uwanja mpira wa miguu na upana wa mita 17 na kimo cha ghorofa nne kwenda juu hii imejengwa na watanzania zaidi ya 200 walioshirikiana na timu ya wataalamu 16 tu wa mkandarasi kutoka Korea” Alisema.
MV New Mwanza ina uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo, magari makubwa 3 pamoja na magari madogo 20. Meli hii imejengwa na Kampuni ya GAS ENTEC CO. LTD ikishirikiana na KANGNAM zote za Korea Kusini pamoja na SUMA JKT kwa gharama ya Shilingi Bilioni 120.