Latest News 16 Jun 2021

Samia: Tunamuenzi JPM miradi ya meli
RAIS Samia Suluhu Hassan amesema mikataba mitano iliyosainiwa jana Mwanza ya ujenzi na ukarabati wa meli ni kazi nzuri ya kumuenzi Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, John Magufuli ambaye ni mwanzilishi wa miradi hiyo.
Aliyasema hayo jijini Mwanza baada ya kuzindua chelezo, meli ya New Victoria ‘Hapa Kazi Tu’ na meli ya New Butiama ‘Hapa Kazi Tu’ pamoja na kushuhudia utiaji saini wa mikataba mitano ya ujenzi wa meli mpya nne na ukarabati wa meli ya zamani.
Rais Samia alisema anajisikia faraja kushuhudia kukamilika kwa ukarabati huo wa meli, kusainiwa kwa mikataba na kukamilika kwa ujenzi wa chelezo.
“Kama ingekuwa haijakamilika roho zetu zisingejisikia vizuri kwa sababu mwanzilishi wa miradi hii ameitwa na Mungu na ameitika, kama anatusikia bila shaka anafarijika,” alisema Rais Samia.
Alisema ni dhamira ya serikali kuifanya Mwanza kuwa kituo kikubwa cha biashara kwa kuwa Mwanza iko kwenye ukanda wa mikoa wazalishaji wakubwa wa mazao wa chakula na biashara na mazao ya uvuvi, hivyo serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji na miundombinu laini ya kuboresha mawasiliano ya kimtandao.
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli, Philemon Bagambilana alisema ukarabati wa meli hizo ulianza Januari 2019 kwa gharama ya Sh bilioni 27.6 na zilianza kufanya kazi tangu Agosti mwaka jana.
Alisema meli ya New Victoria ina uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 200 za mizigo wakati New Butiama ina uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 100 za mizigo.
“Meli ya New Victoria inafanya safari zake mara tatu kwa wiki kati ya Mwanza na Bukoba kupitia Bandari ya Kemondo, na meli ya New Butiama inafanya safari zake kila siku kati ya Mwanza na Nansio Ukerewe,” alisema Bagambilana.
Aliongeza, “Ujenzi wa chelezo nao ulianza Januari 2019 kwa gharama ya shilingi bilioni 36.4, ni chelezo kikubwa kupita vyote katika Ziwa Victoria.”
Alisema meli ya New Victoria ilitengenezwa mwaka 1960 na meli ya New Butiama ni ya mwaka 1980.
Kuhusu mikataba mitano iliyosainiwa, alisema mkataba wa kwanza ulihusu ujenzi wa meli mpya katika Bahari ya Hindi kwa kulenga soko la Comoro na mkataba wa pili unahusu ujenzi wa meli mpya ya mizigo katika Ziwa Victoria itakayokuwa na uwezo wa kubeba tani 3,000 za mizigo kwa kulenga ujio wa Reli ya Kisasa (SGR).
Mingine ni ya ujenzi wa meli mpya ya mizigo katika Ziwa Tanganyika; wa nne ni ujenzi wa meli mpya ya abiria na mizigo katika Ziwa Tanganyika itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo, na mkataba wa tano ulihusu ukarabati wa meli ya Mv Umoja yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na pia ina reli ndani yake.
Bagambilana alisema miradi yote hiyo itagharimu Sh bilioni 438.8.