Latest News 26 Mar 2025

SAMANI ZA MV. MWANZA ZAPOKELEWA JIJINI MWANZA
Siku ya Tarehe 24.03.2025 itabaki kuwa ni siku ya kihistoria baada ya kuwasili kwa makasha 9 yaliyobeba viti 834 vya meli ya MV. Mwanza inayoendelea kuwekewa samani mbalimbali ili kumaliza ujenzi wa meli hiyo unaotarajiwa kukamilika tarehe 31.05.2025.
Wakati akitoa taarifa ya upokeaji wa viti hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya meli Tanzania Wakili Amina Ntibampema alisema kuwa meli hiyo ilianza kujengwa mwaka 2020 baada ya mkataba wake kusainiwa mwaka 2019 na kuongeza kuwa mradi huo ulichelewa baada UVIKO 19 kuleta changamoto ya usafiri na usafirishaji wa vifaa mbalimbali vya meli hiyo.
“Hapa tumepokea kontena 9 za awali zilizotangulia ambazo ndani yake kuna viti vya sehemu ya kukaa abiria tukisubiri shehena nyingine ya vitanda ambapo meli hii itakuwa imekamilika kufikia Mei 31, 2025.”
Mapokezi hayo yaliongozwa na mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi ambaye alisema kuwa mradio huo unaotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TASHICO umegharimu Shilingi Bilioni 123 ambapo mkandarasi ameshalipwa Shilingi bilioni 115.9
“Sasa tunafurahi mradi umefika asilimia 96 na fedha zilizolipwa hadi sasa ni asilimia 93 kama nilivyosema awali, kuwasili kwa samani hizi ni hatua muhimu katika kuelekea kukamilisha mradi huu ambao kwa sasa umefikia asilimia 96 ya utekelezaji wake na ambao unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Mei, 2025.”
Meli hii itakapokamilika itakuwa ndio meli kubwa kuliko zote katika Ziwa hili ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20 na magari makubwa 3.