Latest News 26 Aug 2022
NAIBU WAZIRI MWAKIBETE ATOA MAAGIZO KWA BODI YA MSCL.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Atupele Mwakibete ameiagiza bodi ya Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kuhakikisha wataalamu wa ufundi wa Kampuni hiyo wanashiriki kufanya ukaguzi wa mitambo wakati ikiwa kiwandani inakotengenezwa ili kuepusha changamoto ya kuletewa vifaa vilivyokwishatumika na kuipa serikali hasara.
Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa meli ya MT. Sangara mkoani Kigoma Mhe. Mwakibete alibaini uwepo wa baaadhi ya vifaa vilivyokwishatumika na kusisitiza kuwa Serikali haitaipokea meli hiyo itakapokabidhiwa endapo itagundulika kuwa na mapungufu na hivyo kutoa mwezi mmoja kuhakikisha vifaa hivyo vinaondolewa na kuwekwa vifaa vipya.
“Tunataka ndani ya mwezi huu, viwe vimeshashushwa, sijajua atatumia muda gani ‘ku-order’ lakini ndani ya mwezi wa 9 mpandishe tena hapa, tukija mwezi wa 10 na kuna ziara za viongozi wakubwa katika mkoa wa Kigoma wakija hapa tunategemea tayari spea ziwepo mpya sio tena hizi used, sijui tunaelewana vizuri?” Alisisitiza
Naibu Waziri Mwakibete amesisitiza umuhimu wa watalam kukagua kwa karibu ukarabati huo mkubwa unaofanyika ili kuhakikisha maboresho yote yanayofanyika yanafanywa kwa kufuata vipengele vya mkataba.
Akizungumzia vifaa vinavyotiliwa mashaka Mrakibu wa Meli za MSCL Mhandisi Abel Gwanafyo alisema kuwa kuna vifaa kadhaa ambavyo vinaonekana kuwa vimetumika na mkandarasi tayari ameshaviweka kwenye meli kwaajili ya kutumika.
“Kuna jenereta ya dharura, ipo imepandishwa lakini tunaona kwamba imetumika, tuliikagua, tuliona baadhi ya pump zinaonekana zimetumika, zimekuja injini mbili za kuendesha meli, hizo ni mpya lakini zinakasoro ya kwamba zinazunguka upande mmoja na ‘Gear box’ zake zinazunguka upande mmoja, hiyo tukaona tumsubiri yeye atupe namna atakavyoweza kuziunganisha ili tupate tunachokitaka,” Alieleza.
Meli ya MT. Sangara imefikia asilimia 66 huku Mkandarasi KTMI Co.Ltd ya Korea Kusini akiwa amelipwa asilimia 15 ya gharama za mradi huo ambazo ni sawa na shilingi bilioni 1.2 wakati mradi huo ukigharimu shilingi bilioni 8.4 na unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2022.