Latest News 18 Aug 2022

News Images

MWENYEKITI WA BODI MSCL NA RC KIGOMA WAJADILI USHOROBA WA KATI

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya MSCL Meja Jenerali Mst. John Mbungo amefika kujitambulisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali Mst. Thobias Andengenye mapema leo tarehe 18.8.2022.

Wakati akijitambulisha Mwenyekiti wa Bodi alimshukuru Rais wa awamu ya sita Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua katika nafasi hiyo ili aendelee kuitumikia nchi katika upande wa usafiri na usafirishaji wa njia ya maji kupitia MSCL.

"Pia niendele kumshurukuru Mheshimiwa Rais kwa kuona umuhimu wa kuhuisha miundombinu ya meli ambayo kutokana na ubovu na uchakavu ilisimama kutoa huduma ikiwemo meli ya MV Liemba pamoja na MV Mwongozo, hata hivyo Serikali inampango wa kujenga meli mpya mbili katika Ziwa Tanganyika," alisema.

Kwa upande wake RC Andengenye aliishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kuboresha huduma hizo katika Ziwa Tanganyika huku akisisitiza kuwa maboresho yatakayofanyika ya usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo yatasaidia kuokoa barabara, muda na msafirishaji ataweza kuchagua njia ya kusafirisha mizigo yake.

"Kama usafiri wa ziwani ukiimarishwa kutakuwa hakuna ulazima wa kila mtu kusafirisha mizigo kwa kutumia malori, ukitarajia pengine meli mpaka iende Tunduma, mpaka Zambia halafu ndio iende DRC wakati ingeweza kupitia Karema ama kigoma wanakatiza tu hapa kwenda DRC, ikawa ni rahisi zaidi," alieleza.