Latest News 02 Jun 2022

News Images

Mwenyekiti wa Bodi kuendeleza ndoto za MSCL katika usafiri wa njia ya maji.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Huduma za Meli Meja Jenerali Mstaafu John Mbungo ameridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa meli ya MV Mwanza pamoja na ukarabati wa meli ya MV Umoja na kuahidi kutoa chagizo katika kuhakikisha mafanikio yanakuwa makubwa zaidi.

Ameyasema hayo leo (01.06.20220 mara baada ya kutembelea na kukagua miradi hiyo katika eneo la bandari ya Mwanza Kusini mahala ambapo miradi hiyo inatekelezwa.

“Kwakweli I’m so impressed (nimevutiwa sana) na kazi ambazo zimefanyika na zinazoendelea kufanyika na mimi sasa naahidi kutoa chagizo kubwa katika kuhakikisha mafanikio haya yanakuwa makubwa zaidi,” Alisema.

Aidha, Meja Jenerali Mst. Mbungo alielezea dhamira ya ziara yake hiyo kuwa ni pamoja na kujionea maendeleo yanayofanyika katika ujenzi wa meli za MSCL ambazo serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa cha fedha.

“Nimefika ili kupata nini kinachofanyika na nini kinaendelea lakini pia kuhimiza wenzetu ‘ma-engineer’ (wahandisi) waliopo hapa kwenye ‘site’ (eneo la mradi) waweze kuharakisha, waweze kutumia muda wao vizuri ili kuweza kukamilisha kazi zao mapema kama ambavyo serikali inatarajia meli hizi ziende kuwahudumia wananchi mapema kadiri inavyowezekana,” Alisisitiza.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo ameahidi kuendelea kusimamia majukumu yaliyopo na kuhakikisha MSCL inafanikiwa kwa kiwango kikubwa na matarajio yaliyopo yanafikiwa huku akisifu utendaji kazi wa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu pamoja na menejimenti yake.

“Yapo mabadiliko makubwa, mabadiliko ambayo yanatoa matumaini kwamba tunao mwelekeo mzuri, kampuni hii itakuwa moja ya kampuni kubwa sana nchini ambayo nadhani itakuwa ni sehemu mojawapo ya kujivunia sana kwamba tuna kampuni kubwa inayofanya shughuli zake za usafiri ndani ya maziwa yetu,” Alisema.

Awali Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu Bw. Philemon Bagambilana alisema kuwa ziara hiyo ya siku mbili ni ya kwanza kwa Mwenyekiti huyo wa Bodi na kuongeza kuwa katika ziara hiyo amefanikiwa kuongea na watumishi wa MSCL, menejimenti pamoja na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na MSCL ikiwemo utekelezaji wa miradi ya MV Umoja na MV Mwanza.

Mwisho.