Latest News 25 Jun 2022
MV Umoja yapandishwa Chelezoni
Baada ya siku 201 kupita ambazo ni saw ana miezi sita, wiki mbili na siku sita tangu mkandarasi SM Solution kutoka Korea kukabidhiwa mradi wa Ukarabati wa meli ya MV Umoja, hatimaye meli hiyo imeingia katika hatua ya pili ya ukarabati.
Hatua hiyo hufanyika baada ya ukaguzi wa mwili wa juu pamoja na ukaguzi wa ndani ya meli kukamilika na hivyo kuhamisha ukaguzi huo upande wa chini ya mwili wa meli, ambapo ukaguzi hunafanyika endapo tu meli inapokuwa imepandishwa katika chelezo.
Wakati zoezi hilo likiendelea Kaimu Mhandisi Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) ambaye pia ni meneja mradi wa ukarabati wa meli hiyo Mhandisi Abel Gwananfyo alisema kuwa amefika katika ukaguzi huo mara tu baada ya meli hiyo kupandishwa chelezoni ili kuainisha maeneo ambayo yanahitajika kufanyiwa ukarabati ili kuyapangia mikakati ya namna ya kuyarekebisha maeneo hayo.
“Leo nimepita kukagua kuona meli imekaaje katika chelezo, Je, imekaa katika mstari wake unaotakiwa, maana yake ikikaa pembezoni unaweza ukaiharibu meli, unaipindisha lakini je maeneo ambayo yamedhurika kwa kuyaangalia kwa macho, je, yapo? Ni kweli yapo, meli upande wa kulia imepinda eneo kubwa urefu kama mita 15 na zaidi, imepinda, imebonyea ikionesha kwamba kuna kitu ilikalia,” Alisema.
Hata hivyo, Msimamizi Msaidizi wa Mradi huo upande wa Mkandarasi SM Solution Beda Patrick alisema kuwa kuna baadhi ya vifaa tayari vimeshawasili kwaajili ya kupachikwa katika meli hiyo baada ya zoezi la kuviondoa vifaa vya zamani kufanikiwa.
“Kuna vifaa ambavyo tayari vimeshaingia kama vile vifaa vya mawasiliano pamoja na vifaa vya umeme lakini kuna vingine ambavyo tunavitegemea kuingia hivi karibuni,” Alieleza.
Ikarabati wa meli ya MV umoja unakadiriwa kumalizika mwanzoni mwa mwaka 2023 ambapo itakuwa ikibeba mizigo kutoka Mwanza, Tanzania kuelekea Jinja na Portbell nchini Uganda.