Latest News 07 Sep 2022

News Images

MKURUGENZI MTENDAJI MSCL ASISITIZA NIDHAMU HUKU AKIFIKISHA SALAMU ZA RAIS.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) nchini Ndg. Eric Hamissi amewatahadharisha wafanyakazi wenye tabia ya kukiuka taratibu za miongozo ya utumishi wa umma wawapo eneo la kazi.

Ndg. Eric amesema kuwa kurejea kwake hakujabadili misingi na misimamo yake katika utendaji wa shughuli za serikali na hivyo kuwataka wafanyakazi hao kufanya kazi kwa weledi kwani ameteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuhakikisha kuwa kampuni hiyo inasimama, miradi inakamilika na kuweza kujitegemea.

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, amenileta hapa, anategemea kwamba hii taasisi isimame, miradi ikamilike, iweze kujitegemea, wafanyakazi waneemeke na waongezeke, kwahiyo anataka tukue, haimfurahishi tuwe na hali kama hii siku zote, kwahiyo jitihada anazozifanya za kutoa pesa kwenye miradi tunayoendelea kuitekeleza na mingine minne inakuja, yote ni kuhakikisha kwamba jukumu la hii taasisi ni kujenga uchumi wa nchi,” Alisema.

Aidha ameongeza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutazalisha ajira nyingi nchini pamoja na kutoa huduma stahiki kwa watanzania pamoja nan chi zinazotuzunguka kupitia maziwa tuliyonayo.

“Haitapendeza na haipendezi kuona meli nyingine zinakuja kuchukua mizigo hapa, sisi hatuna hata meli moja ya kuchukua mizigo, kitu kinachoisononesha Serikali na kinanisononesha sana mimi, kwahiyo naomba tuendelee kuungana tupambane kuhakikisha kwamba tunaisimamisha hii taasisi,” Alisisitiza.

Hata hivyo katika kukabiliana na vikwazo vinavyoweza kurudisha nyuma maendeleo ya taasisi, ndg. Eric amesema kuwa hatamuonea haya mfanyakazi yeyote atakayejihusisha na vitendo vya wizi na utovu wa nidhamu mahali pa kazi.

“Sitapenda mnisononeshe,wala mumsononeshe Mheshimiwa Rais, wala muisononeshe Serikali kwa kufanya vitu ambavyo ni tofauti na maadili na matakwa ya utumishi wa umma,”Alimalizia.

Ndg. Eric ameyasema hayo tarehe 31.8.2022 wakati akifunga kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa MSCL ambapo hivi sasa Kampuni hiyo inatekeleza miradi mitatu ya ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza yenye asilimia 71 za utekelezaji, Ukarabati wa meli ya mabehewa ya MV Umoja yenye asilimia 43.5, zote katika Ziwa Victoria pamoja na Ukarabati wa meli ya mafuta ya MT Sangara yenye asilimia 66 katika Ziwa Tanganyika.