Latest News 30 Aug 2022

News Images

MKURUGENZI MTENDAJI MSCL AELEZA MIPANGO YA SERIKALI KUBORESHA USAFIRISHAJI MIZIGO NCHI JIRANI

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) nchini Ndg. Eric Hamissi ameelezea mipango ya Serikali katika kuboresha usafiri na usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es salaam kwenda katika nchi zisizokuwa na milango ya bahari ikiwemo Uganda, Malawi na DR Congo

Ndg. Eric amesema kuwa ndani ya miaka mitatu ijayo MSCL inatarajia kuwa na meli tatu za kubeba mizigo jambo ambalo litaongeza uwezo wa kusafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam kupitia reli na hatimaye kuvushwa na meli za Kampuni hiyo bandari ya Mwanza kwenda Uganda, bandari ya Kigoma kwenda Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo na Bandari ya Kyela kwenda nchini Malawi.

Katika kusisitiza hilo amesema kuwa ukarabati wa meli ya MV Umoja utakapokamilika pamoja na ujenzi wa meli mbili mpya za mizigo katika Ziwa Victoria pamoja na Ziwa Tanganyika utaboresha mapato ya Kampuni hiyo na kufafanua kuwa mzigo unaopita bandari ya Dar es Salaam kwa sasa ni tani milioni 3 ambapo mzigo mwingi unasafirishwa kwa njia ya barabara kwenda katika nchi za Jirani jambo ambalo linachelewesha mizigo hiyo kufika katika nchi hizo.

“Mizigo hiyo kwa sasa inapita kwa njia ya barabara kwenda nchi za DR Congo pamoja na Uganda na hivyo hatuwezi kushindana na mtu mwenye reli, sasa sisi kabla hata ya reli ya SGR, hii reli tuliyonayo tukiijumuisha na water transport (usafiri wa njia ya maji) kwa kutumia wagon ferry (meli za kubeba mizigo) zetu tutapunguza gharama za usafirishaji kwa asilimia si chini ya 40, hivi nani atatumia barabara tena?” Alihoji

Aidha aliwatoa hofu wanaoiogopa bandari ya Mombasa inayopitisha asilimia 98 ya mizigo inayokwenda nchini Uganda ukilinganisha na asilimia 2 inayopita bandari ya Dar es salaam na kuongeza ushirikiano wa MSCL na TPA utatanua wigo wa kusafirisha bidhaa zinazokwenda Uganda kutoka bandari ya Dar es salaam kutoka asilimia 2 zilizopo hadi kufikia asilimia 20.

Ndg. Eric ameyasema hayo jana tarehe 29.08.2022 wakati akifungua kikao cha Kamati Tendaji cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa MSCL ambapo pia alitumia fursa hiyo Kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa MSCL.

Akitoa neno la Shukrani kabla ya kuendelea kwa kikao hicho Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari Tanzania (DOWUTA) Ndg. Edesius Kinunda alimpongeza ndg Eric Hamissi kwa kurejea MSCL na kueleza kuwa alipoteuliwa kwenda TPA, watumishi wengi wa MSCL walihuzunika sana.

“Sina shaka na wewe kwa utendaji lakini nikuhakikishie umeacha kilio kikubwa sana kwa TPA, TPA tangu ilipoanzishwa ikianzia na THA ilipewa maneno mbalimbali kiuzalishaji, lakini utasikia bilioni 400 sijui bilioni ngapi lakini kuja kwako TPA imepata mapato ya Trilioni moja na pointi zake ni historia ambayo haijawahi kuwekwa na DG yoyote aliyewahi kupita TPA,” Alisema.