Latest News 16 Jun 2022

News Images

Maandalizi ya Ukarabati wa meli za MT Ukerewe na MT Nyangumi yaanza.

Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) imewakaribisha wakandarasi kutoka kampuni kadhaa walioomba tenda za ukarabati wa meli za MT Ukerewe pamona ja MT Nyangumi ili kuweza kukagua miundombinu ya meli hizo kabla ya kuwasilisha zabuni zao kwaajili ya kushindanishwa na hatimae kupatikana kinara na kupewa kazi hiyo.

Tenda hizo za meli ya MT Ukerewe inayotumika kusaidia kuvuta meli nyingine ndani ya ziwa pamoja na meli ya mafuta ya MT Nyangumi zitakazofanya shughuli zake katika Ziwa Victoria zilitangazwa mwezi Juni, 2022 katika Mfumo wa Ununuzi wa Njia ya Mtandao Serikalini (TANePS).

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo Mhandisi wa meli wa MSCL Mha. Ester Sikazwe alisema kuwa hatua hiyo ya kuwaalika wakandarasi hao ni hatua za mwanzo kabisa katika mchakato wa kutafuta kampuni itakayoweza kuchukua tenda ya kukarabati meli hizo.

“Walichokuja leo na kilichowaleta ‘site’ (eneo la miradi) ni kuja kujionea kwa macho kwamba kile wanachotaka kuja kukifanyia kazi na walichoambiwa ndio kilivyo, na je, hali halisi ikoje? Hivyo wamekuja kujionea wenyewe,” Mhandisi alisema.

Aidha, aliongeza kuwa wakandarasi hao walipitishwa katika maeneo ya chumba cha kuongozea meli, vyumba vya mabaharia, eneo la injini za meli pamoja na mitambo mingine ya meli kuangalia uchakavu ama kiwango cha ubora wa vyuma vilivyotumika kuundia meli hizo ili kujua uimara wa vifaa vyake tangu viliposimama kutoa huduma zake.Hata hivyo wakandarasi hao hawakuweza kuangalia hali na ubora wa chini ya mwili wa meli hizo.

Akitoa ufafanuzi wa tenda hizo Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi Wilson Zubakwa alisema kuwa nyaraka za zabuni zilizowasilishwa zitapitia katika utaratibu wa ushindani wa kitaifa na kusisitiza kuwa mwisho wa kupokea nyaraka za tenda kwa meli ya mafuta ya MT Nyangumi ni tarehe 07.07.2022 saa 4:00 asubuhi.

“Ukihitaji taarifa za kina zaidi kuhusu tenda hiyo unaweza kutembelea kwenye tovuti ya mfumo wa manunuzi serikalini (www.taneps.go.tz) mkandarasi anatakiwa kujisajili, alipie ada ya ushiriki iliyoelekezwa katika mfumo huo wa manunuzi,” Alieleza.

Fedha za ukarabati wa meli hizo ni kwaajili yam waka wa fedha 2022/2023 na hivyo MSCL inaendelea kuwahamasisha na kuwaalika wazabuni wengine waliosajiliwa katika sekta ya ujenzi wa meli na wakandarasi wa sekta ya usafiri kwa njia ya maji kwa Daraja la pili nakuendelea.

Meli ya Mafuta ya MT Nyangumi iliyojengwa mwaka 1958 in uwezo wa kubeba lita 350,000 huku meli maalum ya kuvuta meli nyingine ya MT Ukerewe ilijengwa mwaka 1983.