Latest News 04 Oct 2019
KONTENA ZAFUNGULIWA,VYUMA VYAANZA KUSHUSHWA RASMI KUANZA KAZI KUUNGA (KUJENGA) MELI KATIKA BANDARI YA MWANZA KUSINI
Vyuma vilivyokatwa maalumu kwa ajili ya kuunganisha(kujenga) Meli Mpya katika Ziwa Victoria vimeanza kushushwa kutoka kwenye shehena ya kwanza ya Kontena 17 zilizowasili nchini kutokea Korea ya Kusini ambako ndiko zoezi la awali la ukataji vyuma hivyo lilikofanyikia.
Kuwasili kwa vyuma hivyo ni ashirio la kukamilika kwa ahadi ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ya Ujenzi wa Meli mpya katika Ziwa Victoria ambayo aliitoa wakati wa Kampeni za uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Naibu waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye alihudhuria katika hafla ndogo ya mapokezi ya Shehena hiyo iliyofanyika katika viunga vya bandari ya Mwanza Kusini tarehe 30 Septemba 2019,akiwa na viongozi wengine akiwemo Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mheshimiwa John Mongella,Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dr.Philis Nyimbi ,Mbunge wa Nyamagana Mheshimiwa Stanslaus Mabula Pamoja na viongozi wengine wa Chama na Serikali
Hatua inayofuata sasa ni kuviunganisha vyuma hivyo ili kuanza kutengeneza umbo la meli (hull) shughuli ambayo itafanyikia katika Chelezo kipya kinachoendelea kujengwa kwenye sehemu maalumu ya kuunganishia vyuma hivyo(Block Assembly) ambayo kwa sasa imeshakamilika kujengwa na kisha kunyanyuliwa na Winchi maalumu kupelekwa katika Chelezo mtelezo (slip way).
Ujenzi wa meli hiyo unatarajiwa kugharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 89 hadi kukamilika kwake ambazo ni fedha za walipa kodi zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.
Mkandarasi wa Ujenzi wa Meli hii ni Kampuni ya GAS ENTEC ya Nchini Korea ya Kusini akishirikiana na Kampuni ya SAEKYUNG nayo pia kutoka Kora ya Kusini pamoja na SUMA JKT ya Tanzania
Ujenzi wa meli hii unatarajiwa kuchukua muda wa miaka miwili hadi kukamilika na kukabidhiwa Serikali(yaani mweziSeptemba 2020).
Itakuwa ni faraja kwa wananchi waishio maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria kwani uwepo wa meli hii utasaidia kufungua fursa nyingi za Kibiashara ndani na nje ya Nchi.
Uwezo wa Meli hiyo ni kubeba abiria 1200 na tani 400 za mizigo na hivyo kuifanya kuwa ni meli kubwa kuliko zote katika Ukanda huu wa Ziwa Victoria