Historia

Kampuni ya Meli Tanzania (Tanzania Shipping Company Limited – TASHICO) ilianzishwa chini ya Sheria ya Makampuni sura 212 mnamo tarehe 08/12/1997 kutokana na kilichokuwa kitengo cha usafirishaji wa majini cha Shirika la Reli (TRC).

Baada ya kuanzishwa ilikuwa ikiitwa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), hadi tarehe 18/11/2024 ilipobadilishwa jina na kuwa TASHICO.

Mali zote zilizokuwa chini ya kitengo cha usafiri majini cha TRC zilihamishiwa katika Kampuni hii mpya mnamo tarehe 21/06/1999 kupitia Gazeti la Serikali No. 125A. Kampuni ilianza kazi tarehe 01/08/1999 ikiwa na mtaji wa meli 15.

Kampuni iliendelea kufanya kazi huku ikimiliki meli, bandari zote na miundombinu yake yote katika maziwa makuu hadi tarehe 30/06/2006. Mnamo mwaka 2004, serikali ilianzisha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari kupitia sheria No. 17 ya 2004. Sheria iliyoanzisha Mamlaka ya Bandari ilianza kutumika tarehe 01/07/2006.

Kutokana na mabadiliko haya baadhi ya mali za Kampuni ya Huduma za Meli ikiwemo miundombinu yote ya kibandari, meli moja, majengo ya ofisi, karakana na vyelezo katika maziwa yote makuu vilihamishiwa Mamlaka ya Bandari Tanzania.

Mabadiliko haya yalipunguza ukubwa na mali za Kampuni pamoja na baadhi ya vyanzo vyake vya mapato.

Kampuni hii kwa sasa inaendesha jumla ya meli 18 za abiria na mizigo, ambapo meli 9 ziko Ziwa Victoria, 3 ziko Ziwa Tanganyika na boti 1 pamoja na 5 ziko Ziwa Nyasa.

Meli 9 za abiria, meli 2 za mafuta, meli 3 za Mizigo, Tug 1, Tishari 2 na Boti 1 ya watalii.

Kampuni hii inaundwa na Matawi matatu; Tawi la Mwanza katika Ziwa Victoria; Tawi la Kigoma katika Ziwa Tanganyika na Tawi la Kyela Katika Ziwa Nyasa. Makao Makuu ya Kampuni yako Mwanza.