Latest News 19 Oct 2022
WAZIRI MKUU AELEKEZA WAHANDISI MV MWANZA KUWEKWA KWENYE KANZI DATA
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezielekeza mamlaka zinazohusika kuhakikisha wanawaweka kwenye kanzi data wahandisi wakitanzania wanaoshiriki katika ujenzi wa meli ya MV Mwanza ili waweze kusaidia katika miradi mingine ya ujenzi wa meli nchini.
Amesema kuwa wakati akitembelea kwenye eneo la injini za meli hiyo alitarifiwa kuwa wapo wahandisi wa kitanzania saba wanaoshughulika na ufungaji wa injini na mitambo mbalimbali ndani ya meli na hivyo kuwataka watanzania kuamini kuwa usalama wa meli hiyo ni mkubwa kutokana na watanzania hao wazalendo kuifanya kazi hiyo.
“Sisi watanzania tunaweza, leo Kampuni hii imekuja unatuamini sisi watanzania kuingia huko ndani kufungasha mitambo, naamini pia usalama wa meli hii ni mkubwa, kwasababu wanaofunga ni wazalendo wa nchi hii, na wanafunga kwa uhakika, hakuna mahali watadanganya ili meli zikianza kazi ule ufundi wao utaaluma wao ushuhudiwe na watanzania.”
“Kama mnataka kujenga boti hizi ndogo ndogo za kwenda Gana, kwenda Irugwa, Irugwa kwenda Nansio, hawa ndio watajenga meli, kwani watashindwa hawa, kama wameujenga mmeli huo mkubwa watashindwa kameli kadogo, tupate orodha ya wale ‘ma-engineer’ wawekwe kwenye kanzi data na wengine muwaajiri kabisa wakae hapa wawe wanakarabati karabati hizi meli,”
Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo tarehe 17.10.2022 alipotembelea na kukagua ujenzi wa meli ya MV Mwanza katika bandari ya Kusini Mwanza na kupokea taarifa ya ujenzi wa meli hiyo katika ziara yake ya siku tatu, Mkoani Mwanza.
Aidha, Waziri Mkuu ameridhishwa na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa meli hiyo na kubainisha imani yake kwa Kampuni ya Gas Entec kuwa itamaliza kazi hiyo kwa wakati huku akisisitiza kuwa nchi ya Korea Kusini na Tanzania ni marafiki na hivyo salamu hizo atazifikisha kwa balozi wa Korea kusini nchini Tanzania pamoja na Waziri Mkuu wa Korea Kusini.
Wakati akitoa taarifa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mha. Godfrey Kasekenya alifafanua kuwa meli hiyo itakapokamilika itakuwa na jumla ya madaraja sita ambapo Daraja la Kwanza litakuwa na watu 60, Daraja la Biashara watu 100, Daraja la Pili watu 200, Daraja la Uchumi watu 834 huku daraja la hadhi ya juu (VIP) watu wanne na vyumba viwili kwa ajili ya watu mashuhuri na hivyo kufanya jumla ya abiria 1,200.
“Mwishoni mwa Novemba meli itatolewa hapo ilipo (kwenye Chelezo) na kuingizwa kwenye maji kwa ajili ya kukamilisha shughuli ambazo zilitakiwa zikamilishwe huku meli ikiwa majini, na mwishoni mwa mwezi wa nne kwenda wa tano meli hii itaanza kufanyiwa majaribio na kama haitakuwa na changamoto itakabidhiwa kwa wahusika MSCL kwa ajili ya kuanza kuiendesha,” Alisema.
Kwa upande wa Meneja Mradi huo Mha. Vitus Mapunda alisema kuwa hadi kufikia tarehe 17.10.2022 ujenzi wa meli hiyo umefikia asilimia 73 huku mkandarasi wa mradi huo akiwa amelipwa asilimia 72 ambazo ni sawa na Shilingi Bilioni 78.