Latest News 07 Sep 2022
RC MALIMA ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA MV MWANZA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amepongeza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza huku akiwasisitiza makandarasi kukamilishaji mradi huo kwa wakati ili kuwanufaisha wananchi waishio kwenye ukanda wa maziwa makuu.
Hayo ameyasema leo tarehe 1.9.2022 baada ya kukagua mradi huo katika bandari ya Mwanza Kusini ambapo hadi meli hiyo itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kubeba magari madogo 20, magari makubwa matatu, tani 400 za mizigo na Abiria 1200 huku thamani ya mradi huo ikiwa ni shilingi bilioni 96.9 na kutekelezwa na Kampuni ya Gas Entec ya nchini Korea.
"Nimefarijika sana leo kuwepo hapa, awali wakati mradi huu unaanza tlipokua ni michoro tu kwenye makaratasi ulikua ukisikia zile takwimu zinatajwa unadhani ni utani, Rais Mama Samia anatengezeza miundombinu kwa ajili ya wananchi wake na hiyo ndio dira ya Mhe Rais wetu ya kuwatumikia wananchi wake na kwakweli ameamua kuhakikisha mambo hayasimami hivyo basi wananchi wa Mwanza wakae mkao wa kusafiri nayo." Alisema.
Wakati akitoa taarifa ya mradi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) Ndg. Eric Hamissi amesema kuwa ni mategemeo kuwa meli hiyo itashushwa kwenye maji mwezi wa Oktoba kwaajili ya matengenezo mengine yanayofanyika ndani ya meli ikiwemo kuweka viti na mifumo mengine.
"Ujenzi wa hii Meli ulianza January 2019 na ulikua uende kwa miaka miwili lakini zilitokea changamoto kadhaa ikiwemo ugonjwa wa Uviko 19 na memngineyo kutokana na hayo mkataba uliongezwa hadi mwezi Mei 2023 ambapo kwa sasa mradi umefikia asilimia 71 na hii ndio meli kubwa katika Ziwa hili na maziwa mengine nchini, hakuna meli kubwa kama hii kwenye ukanda wa maziwa makuu." Alisema.
Vilevile, bwana Hamis ameongeza kuwa ujenzi wa meli hiyo unafanywa na watanzania zaidi ya 200 wakishirikiana na wataalamu 6 kutoka nchini Korea.