Latest News 22 May 2025

News Images

NEW VICTORIA HAPA KAZI TU YAANZA SAFARI ZAKE BAADA YA MABORESHO

Meli ya New Victoria Hapa Kazi Tu inayofanya safari zake za kutoka Mwanza kwenda Bukoba kupitia Kemondo na kutoka Bukoba kwenda Mwanza kupitia Kemondo itarejea katika safari zake za kawaida kuanzia siku ya Alhamisi ya tarehe 22.05.2025

Hayo yemesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Uhusiano kwa Umma Anselm Namala wakati akizungumza na waaandishi wa habari muda mfupi baada ya ziara ya ukaguzi wa meli hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza Ndg. Michael Lushinge Masanja tarehe 20.05.2025.

Namala alisema kuwa meli ya New Victoria inarejea ikiwa na maboresho ya mwendo kasi na mwonekano mpya “Meli hii ambayo ni kipenzi haswa cha wakazi wa kanda ya ziwa ambayo hujulikana zaidi kwa jina la Malkia wa Kanda ya Ziwa, Meli ya New Victoria Hapa Kazi Tu sasa inarejea, na inarejea alhamisi hii tarehe 22.05.2025 iking’oa nanga Bandari ya Mwanza ikielekea Bukoba kupitia bandari ya Kemondo, na hii ni baada ya matengenezo ya takriban miezi miwili.”

Akiongea baada ya ziara ya ukaguzi Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza Ndg. Michael Lushinge Masanja ameishukuru TASHICO kwa kuhakikisha meli inarudi kutoa huduma kwa wananchi kwani ni dhamira ya Rais Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan na wao wasaidizi wake kuhakikisha kero za wananchi zinatatuliwa na kumalizwa.

“Naomba nichukue nafasi hii kwa uongozi wa Kampuni ya Meli kwa kazi kubwa mliyoifanya na namna mlivyoniahidi kuwa meli itakamilika maboresho na itaanza kutoa huduma, leo nimeikagua meli nimeona ina sehemu nzuri za hoteli, Baa na vyumba vya kulala, nawashukuru kwa kuhakikisha meli hii inaanza kutoa huduma,” Alisema.

Aidha, muongoza meli hiyo Nahodha Adam Mwisungu alisema kuwa Meli ya New Victoria Hapa Kazi Tu imeboreshwa eneo la kasi ya meli na hivyo saa za kusafiri zitapungua kutoka saa nane hadi saa saba.