Latest News 18 Aug 2022

News Images

Mwenyekiti wa Bodi MSCL ampongeza Rais Samia miradi ya meli ziwa Tanganyika

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL)Meja Jenerali Mst. John Mbungo amempongeza Rais wa awamu ya sita Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha kwa ajili ya kujenga meli mpya pamoja na kuzikarabati meli zilizokuwa hazitoi huduma kwa wananchi.

Pongezi hizo amezitoa tarehe 17.08.2022 katika ziara yake ya siku moja ya kukagua mradi wa ukarabati wa meli ya kubeba mafuta ya MT Sangara pamoja na kuzitembelea meli ya MV Mwongozo na meli kongwe ya MV Liemba zilizopo katika bandari ya Kigoma, mkoani Kigoma.

“Kwakweli tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuweza kutoa fedha nyingi sana katika miradi hii na kuhakikisha kwamba meli zetu zinakarabatiwa, mbeli ambazo zinahitaji kutoa huduma ndani ya maji haya ya maziwa makuu, zifanye kazi na kuwafikia majirani,” Alisema.

Awali akitoa taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, ndg Philemon Bagambilana alisema kuwa, mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ya Awamu ya Sita imetenga shilingi bilioni 113 kwaajili ya utekelezaji wa ujenzi wa meli huku miradi mitano ikitekelezwa katika Ziwa Tanganyika.

“Katika fedha hizo miradi mitano itatekelezwa Ziwa Tanganyika ikiwemo ujenzi wa chelezo cha kujengea meli maana kilichopo ni kikongwe na ndio kilichotumika kujengea MV Liemba ambacho kina zaidi ya miaka 100, sasa hizi meli kubwa zinazokuja kujengwa, hii miundombinu haiwezi ‘ku-support’ (kuhimili), kwahiyo serikali katika mwaka huu wa fedha itajenga chelezo kipya,”Alielezea.

Miradi mingine inayotarajiwa kutekelezwa katika ziwa Tanganyika ni Ujenzi wa meli mpya ya mizigo itakayokuwa na uwezo wa kubeba tani 3,000. Ujenzi wa meli mpya ya itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo. Ukarabati wa meli ya MV Liemba pamoja na MV Mwongozo ambapo miradi hiyo itagharimu jumla ya shilingi bilioni 45.1.