Latest News 14 Jul 2022

News Images

MSCL KUFANYA JITIHADA ZA KUTATUA UPUNGUFU WA MABAHARIA

Idara ya Utumishi Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) imefanya kikao na mabaharia kwa ajili ya kufahamu uwezo na sifa walizonazo ili kubaini upungufu wa mabaharia wenye sifa stahiki kwa nafasi na ngazi mbalimbali za vyeo katika uendeshaji wa meli.

Aidha, Idara hiyo imewataka mabaharia waliopo kuhakiki taarifa zao na kukusanya vyeti katika idara hiyo kwa wale waliojiendeleza ili kuwekwa katika madaraja wanaostahili kwa kujaza nafasi za ikama za mabaharia wanaotakiwa na Kampuni kabla ya kuangalia mabaharia wenye sifa hizo nje ya Kampuni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mabaharia hao waliorodhesha changamoto kadhaa zinazowasumbua ili idara hiyo iweze kuzifanyia kazi na hatimaye mabaharia wenye sifa kupata stahiki zao kwa maslahi ya Kampuni na kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi bila ya manung’uniko.

Akizungumza katika mkutano huo Afisa Mkuu daraja la pili Bravius Byarugaba aliipongeza idara ya utumishi kwa kufanya kikao na mabaharia ili kujua changamoto zao na hatimaye kuzifanyia kazi na kuwaomba kuendeleza vikao vya iana hiyo ili kuwa na mipango mizuri zaidi ya taasisi.

“Tuwaendeleze waliopo kabla ya kutafuta nje, tuendelee kuwasomesha watu wetu na kuwapatia sea time (muda wa kufanya kazi baharini) ili wawe na sifa kwaajili ya maslahi ya kampuni, kupata watu wenye sifa nje ya Kampuni ni changamoto na waliopo wanaweza kuondoka, ni vyema kuwaendeleza, hii itawapa uzalendo na kupata stahiki zao kuliko kutafuta kazi kwenye maslahi zaidi,” Alisema.

Hata hivyo katika kusisitiza suala la kutafuta watu wenye sifa kwa njia nyepesi katika kada ya ubaharia Mhandisi Mkuu wa meli ya New Victoria Hapa Kazi Tu Alfred Mwingira alisema kuwa si lazima kila baharia aende darasani kwaajili ya kupata mafunzo ya kupata cheti cha Daraja la Nne bali wanaweza kupendekezwa na maafisa wakubwa katika kada hiyo ili wapewe vyeti hivyo.

“Kama hawa mabaharia wanaandikiwa recommendation letter (barua ya kupendekezwa) na maafisa wakongwe wanaotambulikana kuaminika na mamlaka katika kada hii, ni kiasi cha hao mabaharia kufanyiwa mtihani wa Oral (kuhojiwa) na wakifaulu wanapatiwa vyeti na wakaziba hayo ma-gape (mapengo) tuliyonayo,” Alishauri.

Akizungumza katika kikao hicho mkuu wa Idara ya Utumishi Banaga Katabazi alisema kuwa nia na malengo ya kikao hicho ni kusahihisha yaliyopita ili kuweza kuwa na mipango mizuri zaidi ya kuendeleza Kampuni na kulinda maslahi ya mabaharia.

“Mengi tumeyachukua, tutaendelea kuwa na mpango wa mafunzo kwa mabaharia ili kupunguza changamoto ya kutokuwa na watu sahihi kwa wakati sahihi, tutakuwa na mpango wa muda mfupi na muda mrefu kwaajili ya kupunguza malalamiko kwenye maslahi ya kada ya mabaharia, niwatoe wasiwasi kwamba hatutakaa kimya katika kuhakikisha maslahi yanaboreka,” alisema.