Latest News 07 Sep 2022

News Images

KINANA ATAMANI KUIPANDA MV MWANZA

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, amesema ujenzi wa Meli ya MV Mwanza unakwenda vizuri na anatamani kuwa miongoni mwa watu wa kwanza watakaopanda baada ya ujenzi wakekukamilika.

Akiwa katika ziara yakukagua uhai wa Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 jijini mwanza leo Septemba 5, 2022, Kanali Kinana pamoja na mambo mengine ametembelea eneo inapojengwameli hiyo na kueleza ameona hatua kubwa imepigwa.

"Hongereni ndugu wafanyakazi kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya ya kuijenga meli hii na ikikamilika mimi nitakuwa wa kwanza kuja kupanda," amesema akiwa katika eneo hilo la ujenzi wa meli.

Awali akielezea maendeleo ya ujenzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MCSL) Eric Hamissi, amesema kuwa meli hiyo yote imeshaunganishwa na ujenzi umefikia asilimia 71.

"Ujenzi wa meli hii ulitakiwa ukamilike ndani ya miaka miwili lakini chelezo ndio ilichelewa Kukamilika kwani ilikuwa chelezo ianze lakini vilienda pamoja, mradi huu wote unafanyika hapa hapa kwa hiyo tumepata teknolojia mpya. Sasa hivi hatua tuliyofikia na hii meli imebaki kuizindua, kuiweka majini, kuipaka rangi na mwisho wa mwezi wa 10 itaingia kwenye maji, hii ni hatua kubwa sana kwa ujenzi wa meli.

"Itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo na magari 23 makubwa matatu na madogo 20. Meli ni kubwa ina urefu wa mita 92.6,uwanja wa mpira wastan una mita 100, kwa hiyo ni mita 100 toa 92.6, ina urefu wa mita 20 karibu ghorofa nne,” amesema.

“Pia ina upana wa mita 17, ni meli kubwa kuliko meli zote zilizowahi kuelea katika maziwa makuu nchini. Hakuna meli kama hii Kenya, Uganda wa nchi nyingine na hii meli itakuwa na madaraja sita tofauti likiwemo la VIP, itakuwa na uwezo wa kwenda Bukoba kwa saa saba tu tofauti na sasa ambazo hutumia saa 10 hadi 14, kwa hiyo huu ni ukombozi mkubwa," amesema.

Aidha, amesema meli hiyo itakuwa ikifanya safari nje ya Tanzania katika mataifa ya Uganda na Kisumu nchini.