Latest News 14 Dec 2017

News Images

Ofisi ya Kampuni ya Huduma za Meli Yaagizwa Kukamilisha Ukarabati wa Meli kwa Wakati

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ,Mh. John Mongella, ameiagiza Ofisi ya Kampuni ya Huduma za Meli kuhakikisha kazi ya ukarabati wa meli inakamilika kwa wakati ili kuwezesha na kuimarisha shughuli za usafirishaji katika ziwa Victoria.

Aliyasema hayo katika ziara ya kukagua ukarabati wa meli za MV Umoja na MV Crarias katika karakana kuu ya meli ya Mwanza South, Novemba 22, 2017.

"Ukarabati wa meli hizi ufanyike kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma kwa urahisi na Serikali iweze kuingiza mapato", alisema Mh. Mongella.

Awali , Mkuu wa Bandari ya Mwanza Bw. Danie Sila amemueleza Mkuu wa Mkoa kuwa ukarabati huo unaoelekea kukamilika utaimarisha shughuli za usafirishaji na bandari kufanya kazi vizuri zaidi kwa kuwa harakati za kibiashara zitaongezeka na kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo.

Akizungumzia hali ya ukarabati wa meli hizo katika nia ya dhati ya Serikali kuboresha huduma za usafiri katika ziwa Victoria amesema mkazo umewekwa katika ukarabati wa meli hizo za MV Umoja , MV Crarias, MV Butiama na MV Victoria na uundaji wa meli kubwa mpya utakaoanza hivi karibuni kutaboresha kwa kiasi kikubwa huduma za usafiri na usafirishaji katika ziwa Victoria hasa kuanzia Mwanza kwenda maeneo mengine ya ndani na nje ya nchi.

Aidha Mkuu huyo amemshukuru Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa ukarabati wa Meli hizo pamoja na ujenzi wa Meli mpya unaotarajiwa kuanza Mwenzi Januari kwa kuwa Mkandarasi wa kazi hiyo ameshapatikana.

Mkuu wa Mkoa ameshatoa rai kwa wananchi na wanyabiashara kutumia fursa hiyo kuboresha biashara zao kwa kuwa maeneo mengi yatafikika kirahisi na kwa usafiri wa uhakika.

Kaimu Meneja wa Huduma za Meli Mkoa wa Mwanza Bw.Erick B. Hamis ameeleza maendeleo ya ukarabati wa MV Umoja upo katika hatua za mwisho za ukarabati wake na mara ukarabati utakapokamilika basi huduma za usafiri zitaimarika.