Latest News 14 Dec 2017

News Images

Kampuni ya Meli Tanzania Kufanyiwa Mabadiliko

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema atabadilisha uongozi wa menejimenti ya kampuni ya Huduma za Meli Nchini (MSCL), kwa kushindwa kutekeleza uendeshaji na usimamizi wa kampuni hiyo.

Hayo aliyasema katika kikao na wafanyakazi wa kampuni hiyo mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo inayo onyesha kushindwa kujiendesha kibiashara, kuwalipa mishahara wafanyakazi wake na kutoridhishwa na huduma zinazotolewa na MSCL.

“Sijaridhishwa na taarifa za mahesabu yenu katika uendeshaji wa huduma za meli katika ukanda wa Ziwa Viktoria," amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Kwa upande wake Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo, Bw. Erick Hamis, amezitaja changamoto mbalimbali zinazoikabili MSCL, kuwa ni uhaba wa watumishi wenye weledi na ujuzi hususan wenye taaluma ya uhandisi na kukosekana kwa mfumo imara na wakisasa wa udhibiti na ukusanyaji mapato.

“Kampuni inapoteza mapato kutokana na mfumo wa kizamani wa ukusanyaji mapato, fedha nyingi zimekuwa zikipotea na kutumika kusikojulikana, hivyo basi tumeamua kuhakikisha tunaboresha mfumo huu ili kupata mapato zaidi”, amesema Kaimu Meneja Mkuu.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella, ameipongeza serikali kwa hatua iliyochukua ya ukarabati wa meli ya Mv Serengeti ambayo ni msaada mkubwa kwa wakazi wa Bukoba katika usafirishaji bidhaa mbalimbali.

Aidha, amewasihi wafanyakazi kuondoa dhana iliyojengeka ya kufanya kazi kiholela na kwa mazoea na badala kutoa ushirikiano kwa Kaimu Mkuu huyo na Menejimenti itakayoundwa ili kufufua upya kampuni hiyo.